Jumatano , 29th Apr , 2015

Mamlaka ya kudhibiti usafiri wa nchi kavu na majini SUMATRA imesema hakuna sababu ya kuendelea kuwa na vitengo vya kuzuia ajali za barabarani kama ajali zitaendelea kugharimu maisha ya watu kusababisha vifo na vilema vya kudumu.

Mkurugenzi Udhibiti wa Usafiri Barabarani kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) Gilliard Ngewe.

Mkurugenzi wa mamlaka ya usafiri na nchi kavu na majini SUMATRA, Gilliard Ngewe ameyasema hayo mkoani Morogoro wakati akizungumza na wakuu wa jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani kutoka mikoa yote nchini pamoja wa maofisa wa SUMATRA na maofisa wateule wa halmashauri.

Ngewe amesema siku hadi siku ajali za barabarani zimekuwa tishio na zinajenga hofu kwa abiria ambapo zimezitaka mamlaka husika kuhakikisha zinakuwa na mpango madhubuti kwa ajili ya kupambana na ajali hizo vinginevyo hakuna haja ya kuwa na vitengo hivyo.

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani, Mohamed Mpinga akitoa taarifa kuhusu hali ya ajali nchini anasema ajali nyingi zimetokana na makosa ya kibinadamu ambayo yamejumuhisha uzembe wa madereva matumizi mabovu ya barabara ambapo amesema jeshi la polisi litaendelea kujipanga na kutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha ajali zinamalizika.

Katibu Mkuu TAMISEMI, Jumanne Sagini amesema SUMATRA na halmashauri nchini zimefanya makubaliano kutizama upya matumzi ya pikipiki ambapo pamoja na kutoa huduma za usafiri zinatumika vibaya kwa matukio ya uhalifu.