Alhamisi , 31st Mar , 2022

Mbunge wa bunge la Africa Mashariki kutoka Tanzania, Dr. Abdullah Hasnu Makame amesema ujio wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki unasaidia kupanua soko la pamoja kwa wanajumuiya.

Dr Abdullah Hasnu Makame, Mbunge wa bunge la Africa Mashariki

Dr. Makame ameyasema hayo leo kwenye mahojiano na kipindi cha Supa Breakfast cha East Africa Radio ambacho huruka Jumatatu mpaka Ijumaa kuanzia saa 12:00 hadi saa 4:00 Asubuhi ambapo pia amesema Hati ya Kusafiria kwasasa inakuwa ni ya Afrika Mashariki.

''DRC kujiunga EAC ni taarifa nzuri sana kwa wadau na wanajumuiya kwasababu tunazidi kupanua soko la Afrika Mashariki, soko la pamoja ambalo lilikuwa na watu takribani Mil 170, sasa wanaongezeka Mil 100 kwahiyo inakuwa Mil 270,'' amesema Dr Abdullah Hasnu Makame, Mbunge wa bunge la Africa Mashariki.

Aidha amesisitiza kuwa, ''Kwasasa ukiomba Hati ya Kusafiria utapewa na Mamlaka yetu ya Uhamiaji lakini inakuwa ni ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwahiyo utasafiri Nchi hizo kama kawaida''.

Pia ameongeza kuwa, ''Haimanishi kwamba watu watakwenda na kurudi DRC kiholela, lazima taratibu zifuatwe ikiwemo Hati ya kusafiri na masharti yote ya kusafiri, kama ikihitajika mtu awe amechanja chanjo ya Uviko-19 au Homa ya manjano atafanya hivyo''.