Alhamisi , 24th Dec , 2015

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemalizia kujaza nafasi za uteuzi wa mawaziri na Naibu Waziri alizobakiza wakati akitangaza baraza la mawaziri la kwanza katika awamu ya tano ya utawala wake.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongea jana wakati akitangaza uteuzi wa Mawaziri waliobaki baada ya uteuzi wa kwanza.

Katika uteuzi huo Dkt. Magufuli amemteua Profesa Jumanne Maghembe Waziri wa Maliasili na Utalii , Dkt. Philip Mpango ameteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango baada ya kumteua kuwa mbunge, Mhandisi Gerson Lwenge ameteuliwa kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji.

Aidha Dkt. Joyce Ndalichako ameteuliwa kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, baada ya kumteua kuwa mbunge huku Prof. Makame Mbarawa akumuhamisha kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji na kwenda Wizara ya Ujenzi, uchukuzi na Mawasiliano.

Pia Dkt. Magufuli amemalizia nafasi ya Naibu Waziri wa Mambo ya ndani kwa kumteua Mheshimiwa Hamad Masauni kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Dkt. Magufuli ameongeza kuwa baada ya kumteua Dkt. Mpango kuwa waziri amemteua ndugu Kadata kuwa Kaimu Kamishana wa Mamlaka ya mapato nchini TRA, mpaka hapo atakapofanya uteuzi mwingine.

Katika hatua nyingine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewatakia heri watanzania wote katika Sikukuu za Maulid, Christmas na Mwaka Mpya na kuwataka washerehekee kwa amani na utulivu.