Jumatatu , 13th Mei , 2024

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia mtu mmoja, Yahaya Mohamed (28), Dereva wa gari lenye namba za usaji T 736 AXN aina ya Mitsubishi Fuso kwa tuhuma za kusababisha ajali iliyogharimu maisha ya watu watano na majeruhi mmoja.

Fuso

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema ajali hiyo ilitokea jana Mei 12, 2024, saa 1:30 usiku katika barabara kuu ya Mwanga – Same, eneo la Lembeni, Wilaya ya Mwanga.

Kwa mujibu wa Kamanda Maigwa, Fuso alilokuwa akiendesha dereva huyo, liliacha barabara na kuparamia watu sita waliokuwa kando ya barabara wakiwa hawana hili wala lile.

Watu hao walikuwa ni abiria wa gari namba T 122 DGM Toyota Coaster ambalo lilikuwa limeharibika na kuegeshwa kando ya barabara hiyo kwa matengenezo.

"Abiria hao walikuwa nje ya gari wakisubiri matengenezo ya gari hilo... Baada ya ajali hiyo, watu watano walifariki dunia papo hapo kati ya sita waliogongwa," amesema Kamanda Maigwa

Amewataja waliopoteza maisha kuwa ni Cosmas Severine, mkazi wa Mbezi; Jackline Mushi, Mkazi Moshi Karanga; Dorothea Masawe, Mkazi wa Mbezi; Hiza Hamisi, Mkazi wa Mwanga na Lucasia Otaru, Mkazi wa Moshi.

Aidha Kamanda amesema majeruhi mmoja, Christiani Kiwango amevunjika mguu wa kushoto na amelazwa katika Hospitali ya KCMC.

Kamanda Maigwa amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na uzembe wa dereva huyo kwa kushindwa kuchukua tahadhari kwenye mteremko mkali wenye kona.

Ametoa wito kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara kuongeza umakini na hasa nyakati za usiku.