
Pichani dawa za kulevya, zikiwa zimefungwa tayari kwa kwenda kuteketezwa
Zoezi la kuangamiza dawa hizo limefanyika katika jaa la Kibele, Wilayaya Kati, Kabla ya hatua ya kuzingamiza, dawa hizo zilikuwa zikitumika kama vielelezo vya ushahidi katika mahakama na vituo vya polisi kisiwani Unguja, ambapo sasa kesi zake zimemalizika na kutolewa hukumu.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kuangamiza dawa za kulevya ambae pia ni Mfamasia Mkuu wa Serikali Habibu Ali Sharif, amesema zoezi hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa na hakuna athari yoyote iliyotokea wakati lilipotekelezwa.
“kamati yangu inaendelea kuangalia uwezekano wa kuangamiza dawa kama hizi hapo baadae katika sehemu zilikopatikana badala ya kuzipeleka kwenye jaa la Kibele”, amesema Mfamasia.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Abdalla Hassan Mitawi, amesema serikali imekuwa ikichukua hatua za kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria watu wanaoingiza, kusambaza na kuuza dawa hizo hatari ili kukinusuru kizazi cha sasa na baadae.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Kheriyangu Mgeni Khamis, amesema zoezi hilo ni la pili kufanyika ambapo mwezi uliopita kamati iliangamiza dawa za kulevya aina ya bangi. Zoezi la uangamizaji dawa za kulevya linakwenda sambamba na maadhimisho ya siku ya kupambana na dawa za kulevya duniani inayofikia kilele Juni 26, 2018.