Jumapili , 9th Nov , 2014

Chama cha wananchi CUF kimeitaka serikali kutafuta suluhu ya haraka ya ukosefu wa dawa katika hospitali za umma kwa kuwa zaidi ya 75% ya watanzania wanaathirika na hali hiyo.

Chama cha wananchi CUF kimeitaka serikali kutafuta suluhu ya haraka ya ukosefu wa dawa katika hospitali za umma kwa kuwa zaidi ya 75% ya watanzania wanaathirika na hali hiyo.

CUF kimesema watu wenye ulemavu, wazee, wajawazito, pamoja na watoto wadogo ndio waathirika wakuu wa tatizo la ukosefu wa dawa katika hospitali na vituo vya afya vya umma.

Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba, amesema hayo leo wakati akizungumzia ukosefu wa dawa katika hospitali za umma, kutokana na Bohari ya dawa – MSD, kushindwa kusambaza dawa na vifaa tiba kutokana na deni kubwa ambalo bohari hiyo inaidai serikali.

Kwa upande wake, mratibu wa shirikisho la vyama vya watabibu wa tiba asilia nchini Tanzania Bw. Boniventura Mwalongo amesema kama nchi kuna haja ya kuchukua hatua kukabiliana na uhaba wa dawa badala ya kila mtu kuendelea kulalamika.

Amesema afya ya watanzania kuwekwa mikononi mwa wahisani ni changamoto kwa taifa kufikiria njia mpya ya kutafuta suluhu ya upungufu wa dawa.

Kwa mujibu wa Mwalongo, kuna haja ya viongozi kuwaeleza watanzania umuhimu wa kutafuta nafuu ya magonjwa yanayowasumbua kwa kutumia tiba asilia, kama mbadala wa tatizo la ukosefu wa madawa hospitalini.