Jumanne , 2nd Feb , 2016

BAKWATA mkoa wa Dar es salaam imewataka wazanzibari pamoja na vyama vyote vya siasa visiwani humo kushiriki uchaguzi mkuu wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe 20 mwezi Machi mwaka huu.

Baraza Kuu la Waisilamu BAKWATA mkoa wa Dar es salaam limewataka wazanzibari pamoja na vyama vyote vya siasa visiwani humo kushiriki uchaguzi mkuu wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe 20 mwezi Machi mwaka huu ili kumaliza mvutano wa kisiasa unaoendelea visiwani humo hivi sasa.

Kauli hiyo imetolewa leo na Sheikh wa Mkoa wa Dar es salaam Sheikh Alhad Mussa Salum, wakati akiongea na waandishi wa habari na kuongeza kuwa hakuna njia mbadala ya kuutatua mgogoro huo kwa hivi sasa zaidi ya kurudia uchaguzi huo kwa amani ili wananchi waweze kumpata kiongozi waliomchagua kwa kufuata sheria na kanuni.

Aidha Sheikh Salum amebainisha kuwa hata kiongozi wa uamsho Sheik Amir Hadi Ahmadi pia anaunga mkono suala la kufanya uchaguzi wa marudio kwa mujibu wa barua yake alioituma kwa sheikh wa mkoa wakati kiongozi huyo akiwa gerezani.

Kuhusu uamuzi wa Chama cha Wananchi CUF kususia uchaguzi huo, baraza hilo limesema linaunga mkono uamuzi wa ZEC, na kukiomba chama cha CUF kukubali kurudia uchaguzi, ili kutatua mgogoro huo.

“Kuhusiana na suala la mgogoro uliopo Zanzibar, sisi BAKWATA MKOA WA DAR ES SALAAM, tunaunga mkono uamuzi wa Tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuamua kufanya uchaguzi wa marudio, hivyo basi naomba kuchukua fursa hii kukiomba chama cha Wananchi CUF ambacho kimeshatangaza kususia uchaguzi huo, viache kususia uchaguzi huo bali vijipange na kushiriki”, alisema Sheikh Salum.

Baraza hilo pia limewaomba wazanzibari wote waendelee kudumisha amani na utulivu walionao ili kulinda umoja na mshikamano walionao kwa hivi sasa kwani wakikubali kuipoteza amani hiyo ni ngumu sana kuirudisha.

Aidha baraza hilo limeipongeza serikali ya awamu ya tano kwa jitihada mbalimbali inazofanya za kuimarisha nidhamu, kubana matumizi na kukuza uchumi.

“Kusudi kubwa la kuwaiteni leo ni kutaka kutoa salamu za pongezi kwa serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Mh. John Magufuli, kutokana na hatua mbalimbali inazozichukua zenye lengo la kuimarisha nidhamu hasa kwa watumishi wa umma, hatua mabazo zimeanza kuleta tija kubwa ka taifa letu kama wote hivi leo tunavyoweza kushuhudia jinsi pato la serikali likongezeka mwezi hadi mwezi”, alisema Sheikh Alhad Mussa Salum ambaye ndiye sheikh wa mkoa wa Dar es salaam.

Pia Baraza hilo limeipongeza serikali kwa kitendo cha kubana matumizi na kuweka kipaumbele huduma za jamii, kama suala la elimu bure.

“Aidha tunaipongeza kwa dhamira yake ya kubana na kupunguza matumizi ya serikali, na badala yake kuelekeza fedha kwenye huduma za jamii na watanzania tumeshaanza kunufaika na huduma hizo kama vile suala la elimu bure”, alisema Sheikh Salum.

Vile vile Baraza hilo limeitaka serikali kushughulikia changamoto za jiji la Dar es salaam ikiwemo tatizo la foleni, kwani linazorotesha uchumi pale wafanyakazi wanapochelewa sehemu zao za kazi, na kuomba kuanza kutumika kwa mabasi ya mwendo kasi ili kupunguza tatizo hili.

sheikh Mussa Salum alipokuwa kwenye mkutano na wandishi wa habari (hawapo pichani)