Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na taasisi mbili kubwa za kimataifa jana, Jumapili, Oktoba 26, 2014, zilitiliana saini Hati ya Makubaliano (MOU) ya kuendeleza kwa pamoja Eneo la Kiuchumi la Bagamoyo ambako pia itajengwa bandari kubwa ya Bagamoyo ambayo inatarajiwa kutoa mchango mkubwa kwa uchumi wa Tanzania.
Pande hizo tatu ambazo ni pamoja na Kampuni ya Uendeshaji Bandari ya China Merchant Holding International (CMHI) ya Jamhuri ya Watu wa China na Mfuko wa Uwekezaji wa Oman wa State General Reserve Fund of Oman ya Oman zimetilia saini Hati hiyo kwenye sherehe iliyofanyika katika Hoteli ya Hilton Shenzhen Shekou Nahai ya mjini Shenzhen, Kusini mwa China.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ametembelea Jimbo la Guang Dong ambako liko Eneo la Uwekezaji wa Kiuchumi la Shenzhen alishuhudia utiaji saini huo ambao kwa upande wa Tanzania saini ilitiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Servicus Likwelile.
Chini ya Hati hiyo ya uendelezaji wa Eneo la Uwekezaji la Bagamoyo litaanza kujengwa Julai Mosi mwakani, 2015.
Kabla ya sherehe hiyo ya kutiliana saini Hati ya Makubaliano, Rais Kikwete ametembelea Eneo la Kontena la Bandari ya Shenzhen ambako alionyeshwa vifaa vya kisasa kabisa vya kupakia na kupakulia kontena kazi inayofanywa na CMHI ambayo ina uzoefu wa miaka 140 wa uendeshaji wa bandari.
Akizungumza katika sherehe hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake imedhamiria kuhakikisha kuwa mradi huo wa mamilioni ya fedha wa Bangamoyo unaanza. “Tutafanya lolote linalowezekana kuhakikisha kuwa mradi huu unaanza kwa sababu utaleta neema kubwa ya kiuchumi kwa nchi nzima.”
Naye Mwenyekiti wa CMHI, Bwana Li Jianhong ameitaka Serikali kuangalia uwezekano wa kumaliza vikwazo vyote ambavyo vimechelewesha kuanzishwa kwa mradi huo ili uweze kuanza Julai Mosi, mwakani, kama ilivyokubaliwa.
Mapema leo akiwa Shenzhen, Rais Kikwete ametembelea makao makuu ya Kampuni ya Teknolojia ya Mawasiliano ya Hauwei Technologies inayoajiri maelfu ya watu duniani, ikiwemo Tanzania, na kutengeneza mamilioni ya faida.
Aidha, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Manispaa ya Shenzhen ambayo yalifanyika kwenye hoteli ambako alifikia Rais Kikwete katika ziara yake ya Shenzhen ya Shenzhen Wazhou Guest Hotel ambayo ni mali ya Serikali ya China.
Rais pia ametembelea Makao Makuu ya Kampuni ya Teknolojia ya Mawasiliano ya ZTE iliyoko mjini Shenzhen ambayo inaendesha shughuli zake Tanzania na inaajiri wafanyakazi 60,000 dunia nzima.
Rais Kikwete amemaliza ziara ya China jana, naleo, Jumatatu, Oktoba 27, anaanza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku mbili katika Vietnam.