Marehemu Alphonce Mawazo enzi za uhai wake.
Marehemu Mawazo amefariki baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana, tukio lililotokea eneo la Ludete mkoani Geita hapo jana.
Mbowe amesema kuwa kwa niaba ya viongozi na wanachama wote wa CHADEMA, ametuma salaam za pole na rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, wanachama wa CHADEMA na wote walioguswa na kifo hicho cha kikatili, huku akivitaka vyombo vya dola vitoe taarifa kamili ya wahusika wa unyama huo.
Mbowe amemwelezea Mawazo kwama mmoja wa wapiganaji jasiri na makini ambao watanzania wapenda mabadiliko walikuwa wakijivunia kuwa naye. "Hakika tumepoteza moja ya nguzo muhimu za chama Kanda ya Ziwa. Chama kimepokea kwa mshtuko mkubwa kifo hiki ambacho tunaamini kimepangwa." alisema Mbowe.
Ameongeza kuwa "Tunavitaka vyombo vya dola vitupe taarifa kamili ya wahusika wa unyama huu. Nawapa pole Wanachadema wote, ndugu na jamaa," amesema Mwenyekiti Mbowe katika taarifa yake ya kuomboleza kifo hicho.
Mbali ya kuwa mwenyekiti wa chama mkoa wa Geita, Mawazo pia alikuwa Mjumbe wa Baraza Kuu na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Taifa.