Alhamisi , 4th Dec , 2014

Wanachama na viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, wilayani Arumeru Mkoani Arusha wameiomba Tume ya Uchaguzi kuacha kufumbia macho malalamiko yanayotolewa dhidi ya baadhi ya watendaji wa vijiji na Mitaa.

Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kupitia Chadema Mh. Joshua Nassari.

Wananchi hao wametoa ombi hilo walipokuwa wanazungumzia hatua ya wagombea wao zaidi 68 waliowekewa pingamizi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo zilizoko nje ya uwezo wao na wamelalamika kuwa wamekuwa hawapati ushirikiano toka kwa waliopewa dhamana ya kusimamia zoezi hilo.

Mbunge wa Jimbo hilo Mh. Joshua Nassari amesema pamoja na jitihada za wanachama wao za kutimiza vigezo vya tume ya uchaguzi na pia kukata rufaa wengi wao bado wamekwama na kwamba kama tatizo hilo halitatatuliwa mapema linaweza kuleta majanga baadaye na amesisitiza umuhimu wa ngazi zinazohusika kufuatilia na kuchukua hatua.

Baadhi ya waratibu wa zoezi hilo akiwemo Katibu Tawala wa Wilaya ya Arumeru Evalilian Boma amesema wanaendelea kutatua changamoto zinazojitokeza na amewaomba wananchi na wagombea kuendelea kutoa ushirikiano.