Ijumaa , 8th Dec , 2017

Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimewataka Wabunge wake ambao ni sehemu ya Timu ya Michezo ya Bunge la Tanzania, inayoshiriki michezo ya Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wote wa wajitoe mara moja

kwenye kambi ya timu hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano CHADEMA, Tumaini Makene amesema kwamba maadhimio hayo awali  yametolewa baada ya Kamati Kuu kupokea taarifa na tathmini ya kina ya uchaguzi wa marudio katika kata 43 uliofanyika hivi karibuni, ambao ulitawaliwa na uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu, vitendo vya kinyama dhidi ya ubinadamu 

Taarifa hiyo imesema kwamba baada ya Kamati  kujiridhisha kuwa vitendo hivyo vimefanyika kwa makusudi, vikilindwa au kunyamaziwa na mamlaka za kiserikali zenye wajibu wa kusimamia taratibu za uchaguzi, vikiwemo vyombo vya dola, lengo ikiwa ni kutaka kuua siasa za ushindani wa vyama vingi na kipekee kuishughulikia CHADEMA, wanachama, wafuasi, mashabiki na viongozi wake.

"Wabunge wote wa CHADEMA ambao ni sehemu ya Timu ya Michezo ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoshiriki michezo ya Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) waondoke mara moja kwenye kambi ya timu hiyo. Wajitoe rasmi kushiriki mashindano hayo ambayo mwaka huu Tanzania ndiyo nchi mwenyeji, yakifanyika jijini Dar es Salaam" Kauli ya Kamati.