Jumanne , 16th Dec , 2014

Chama cha Mapinduzi CCM kimesema hakioni sababu ya suala la waliohusika kusababisha dosari zilizojitokeza wakati wa zoezi la upigaji kura kuundiwa tume au kuchunguzwa wakati wanajulikana.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye

Chama hicho kimesema kuwa badala ya hatua hizo, watu hao wachukuliwe hatua, huku kikieleza kusikitishwa na mapungufu yaliyojitokeza ambayo wamedai yalitokana na uzembe wa watendaji wachache.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho Bw Nape Nnauye ameyasema hayo jijini Dar es Salaam ambapo amesema wakati umefika utaratibu wa kuunda tume kila jambo ufe kwani ni matumizi mabaya ya fedha na mwisho wa siku zinaleta ripoti wakati machungu ya jambo yakiwa yameisha hivyo haifanyiwi kazi tena huku akielezea namna CCM ilivyofanya vizuri katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Aidha kwa mara ya kwanza Bw Nape amevipongeza vyama vya upinzani kwa hatua vilivyofikia lakini akadai kuwa kwa umri waliofikia tangu vianzishwe hapa nchini havikupaswa kuwa hatua vilivyopo hivi sasa bali walitakiwa kuwa mbele zaidi huku akivitaka kutekeleza yale yote waliyoahidi kwa wananchi waliowapa dhamana na kuongeza kuwa furaha ya CCM ni kuona mfumo wa ushindani unakua.