Jumanne , 26th Jul , 2016

Kamati ya Umoja wa Mataifa inayopinga utesaji CAT, imeanza vikao nchini Uswisi, kujadili hatua zilizochukuliwa na mataifa mbalimbali za kisheria dhidi ya watu waliohusika na vitendo vya utesaji vilivyofanyika katika nchi hizo

Askari nchini Burundi wakiwa katika harakati za kutuliza Ghasia.

Kamati hiyo inatarajia kufanya tathimini maalum kuhusu Burundi, kufuatia taarifa ambazo imekuwa ikipokea za kuzorota kwa haki za binadamu nchini humo.

Julai 28 hadi 29 wajumbe wa CAT pamoja na ujumbe wa Burundi ukiongozwa na waziri wa sheria, watajadili mambo kadhaa ambayo kamati iliomba ripoti hiyo mwaka jana Desemba kutoka kwa serikali ya taifa hilo linalokabiliwa na machafuko.

Miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa ni pamoja na hatua zilizochukuliwa kuchunguza mauaji, uwekwaji vizuizini, utesaji na matibabu kwa wanachama wa upinzani.

Kadhalika kamati hiyo ya kupinga utesaji CAT na wajumbe wa serikali ya Burundi watajadili hatua zilizofikiwa katika uchunguzi wa mashambulizi dhidi ya mwanaharakati wa haki za binadamu Pierre-Claver Mbonimpa mwezi Agosti mwaka jana pamoja na kutekwa na kuawa kwa mwanae Welly Nzitonda mwezi Novemba mwaka huo huo.