Jeneza lenye mwili wa Bernard Membe likiwekwa kwenye makazi yake ya milele
Haukuwa urafiki tu, bali ni umakini kwenye kazi na kutegemeana kwa kila hali, naam Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt Jakaya Kikwete anaeleza kwa majonzi makubwa kwa kumpoteza rafiki lakini mtu muhimu aliyemfaa hata kwenye ushauri.
Malengo ni kuendeleza alivyoanzisha na kuyaishi maisha yake kama ambavyo yeye ingempendeza, viongozi wengine akiwamo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wamepanga kulisimamia hilo huku wakikiri kuumizwa na msiba huo.
Familia, Watanzania na wana Rondo leo hii wamemsindikiza mpendwa wao Benard Membe kwenye makazi yake ya milele. Sauti za vilio na macho yanayobubujikwa na machozi ni alama dhahiri kwamba mwanadiplomasia huyu imara ameliacha pengo.
Bernard Membe amefariki dunia Mei 12, 2023, katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Hubert Kairuki jijini Dar es Salaam baada ya kupata maambukizi ya ghafla ya mapafu yaliyopelekea damu kuganda.