Jumatano , 7th Aug , 2019

Kamanda wa polisi Mkoa wa Shinyanga Richard Abwao, amesema watu wasiojulikana wamevamia na kumuua mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Hamis Kadilanha Salehe, tukio lililotekea Agosti 6,2019 majira ya saa mbili usiku, ambapo watu wapatao watano walitekeleza mauaji hayo na kujeruhi

watu wawili.

Mtu huyo aliyeuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali ni mkazi wa kijiji cha Nyambula kata ya Ngogwa, Halmashauri ya mji wa Kahama aliyekuwa amelala ndani na mkewe Shija Mkela Maziku ambaye yeye alijeruhiwa.

"Chanzo cha tukio hilo kinasadikiwa ni imani za kishirikina, kutokana na tukio la kupigwa na radi mwezi wa Februari, 2019 ambapo ilisababisha kifo cha mdogo wake na marehemu aitwaye Mhoja Kadilanha Salehe (45), mkazi wa Nyambula pamoja na mkewe aitwaye Pili Tabu Mabula (36), mkazi wa Nyambula na wakati wengine waliokuwa pamoja nao hawakupata madhara kutokana na radi hiyo", amesema Kamanda Abwao.

Kamanda ameitaja mbinu waliyotumia waharifu hao  ni kuvunja mlango na kumvamia akiwa amelala chumbani kwake na mkewe, ambapo mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Halmashauri Mji wa Kahama.