Jumatatu , 25th Aug , 2014

Viongozi wa serikali na vyama vya siasa nchini Tanzania wametahadharishwa kuwa makini na suala la mchakato wa Katiba mpya, kutokana na suala hilo kuwa na mgawanyo wa makundi ambayo yanaweza kuvuruga umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

Wafuasi wa chama cha upinzani cha Alliance for Democratic Change ADC wakifurahia mara baada ya chama hicho kupata usajili wa kudumu.

Mwenyekiti wa Chama cha siasa cha Alliance For Democratic Change ADC Bw. Said Miraji amesema iwapo viongozi hawatakuwa makini na suala la Katiba mpya linaweza kuvuruga amani ya nchi kutokana na kila kundi kuwa na malengo yake binafsi katika mchakato wa upatikanaji wa Katiba hiyo.

Amesema makundi hayo yanaweza kuhatarisha amani kwa kuwajaza wananchi chuki kuhusu mchakato wa katiba mpya hivyo ni vyema suala hilo likaangaliwa na kuchukuliwa tahadhari mapema kabla ya kutokea kwa hali ya sintofahamu.

Wakati huo huo, Msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania Jaji Francis Mutungi ameombwa kushughulikia na kumaliza mgogoro unaokikabili chama cha siasa cha upinzani cha (TADEA).

Mmoja wa waasisi wa chama hicho Mzee Joachim Mwingira amesema hayo leo wakati alipokuwa akizungumzia mgogoro unaokikabili chama hicho ambapo pia ameshauri vijana kujiunga na chama hicho kwa ajili ya kugombea nyadhifa mbali mbali za uongozi.

Amesema kwa sasa chama hicho kina mvurugano unaotokana na mgongano wa kimaslahi baina ya viongozi waliopo kwa sasa jambo ambalo amesema kama msajili ataingilia kati linaweza likamalizika na chama kuwa na muonekano mzuri kwa wanachama wake na jamii kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Chama cha Demokrasia na maendeleo nchini Tanzania Chadema kimetangaza kusogeza mbele muda wa kurudisha fomu kwa wagombea wa nyadhifa mbalimbali za uongozi wa chama hicho ikiwemo ngazi ya taifa hadi kufikia Agosti 30 mwaka huu.

Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na usimamizi wa Kanda wa chama hicho Bw. Singo Bensoni amesema lengo ni kuhakikisha vijana na watu wengi wanashiriki uchaguzi huo kwa kugombea nyadhifa hizo.

Kwa upande wake Mmoja wa wagombea wa nafasi ya Uenyekiti katika Baraza la Taifa la Vijana la Chadema Bi. Upendo Peneza amewaasa vijana kushiriki chaguzi hizo kwa lengo la kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kuachana na dhana kwamba masuala ya kisiasa ni kwa ajili ya wazee pekee.