
Jeshi la polisi limekamata watu watatu kwa tuhuma za kuharibu miundombinu ya mabasi ya mwendokasi huku likiendelea kuwasaka wengine walioshiriki katika tukio hilo.
Watu hao wanatuhumiwa kwa kuyashambulia kwa mawe mabasi yaendayo haraka (Mwendokasi) usiku wa Oktoba 1 majira ya saa mbili usiku maeneo Gerezani Kariakoo, Magomeni Mapipa, Magomeni Usalama na Magomeni Kagera kwenye vituo vya mabasi ya mwendokasi baadhi ya mabasi yalirushiwa mawe na vituo hivyo baadhi vioo vyake kuvunjwa.
Imeelezwa kuwa kando na mabasi hayo, vituo vya abiria wa magari hayo maarufu kama vituo vya mwendokasi vilishambuliwa pia na vioo vya magari na vituo kupasuliwa.
Video zilizoenea katika mitandao ya kijamii zilionyesha hali ya vituo hivyo, huku sababu ikiwa haijajulikani ya watu hao kushambulia vituo na magari hayo.
Jeshi la polisi limesema bado linachunguza chanzo cha tukio hilo na limetoa onyo kwa watu kutojihusisha na uharibifu wa miundombinu ya umma.