Jeshi la Polisi limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi wa Dumila na Mbigiri wilayani Kilosa mkoani Morogoro baada ya kufunga barabara ya Morogoro Dodoma kwa kutumia mawe na kuchoma matairi barabarani katika eneo la Dumila na kusababisha abiria wanaotumia barabara ya Morogoro Dodoma kukosa mawasiliano kwa zaidi ya masaa sita.
EATV imeshuhudia wananchi hao wakifunga barabara kwa mawe na matairi huku wengine wakionekana na mapanga ambapo wamesema wanalalamikia viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya kijiji hadi wilaya kufumbia macho mgogoro wa ardhi na kushindwa kuwachukulia hatua wafugaji wanaowazuia wakulima wasilime katika eneo la Mbigiri.
Vurugu hizo zilidumu kwa muda mrefu na juhudi za kudhibiti wakulima hao zimechukua muda baada ya askari wachache wa kituo cha Dumila kuonekana kuzidiwa nguvu ambapo baadhi ya wakulima wengine wameonekana wakivamia na kuvunja nyumba za wageni zinazomilikiwa na wafugaji na kupora magodoro na vitu mbalimbali ambapo baadaye vikosi vya jeshi la polisi viliongezwa na kufanikiwa kudhibiti baadhi ya watuhumiwa na kufungua barabara.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro Lenard Paul amesema chanzo cha vurugu hizo ni wazee zaidi ya kumi walizuiwa kulima katika mashamba yao Mbigiri ambapo walipelekeka malalamiko yao kwa afisa tarafa ambapo wakiwa ofisini kundi la vijana walifika na kufunga ofisi wazee hao pamoja na afisa tarafa hadi walipofika na kuokolewa na jeshi la polisi na katika tukio hilo watu 20 wanashikiliwa na jeshi la polisi.
Afisa tarafa na wazee walifungiwa ndani wakizungumzia tukio hilo wamesema kuna mgogoro wa siku nyingi kati ya wakulima na wafugaji na upo katika ngazi za juu huku wakieleza kusikitishwa na hatua za kufunga barabara na kuomba serikali kuingilia kati kutatua mgogoro wa ardhi uliopo.