Vikosi vya usalama vikikabiliana na waandamanaji wanaopinga rais Pierre Nkurunziza kuwani urais kwa awamu ya tatu huko nchini Burundi.
Msemaji wa wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Issac Nantanga, amesema hayo leo wakati East Africa Radio ilipotaka kufahamu idadi kamili ya raia wa Burundi waliopo nchini na hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuhakikisha kuwa uwepo wao hauhatarishi amani ya nchi.
Nantanga amesema zoezi la kuwatambua na kuwahifadhi wahamiaji hao limekuwa likifanywa kwa ushirikiano nashirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi la UNHCR, huku akiweka wazi kuwa Tanzania kwa sasa haina mpango wa kuhifadhi na kuhudumia wakimbizi.
Kwa mujibu wa Nantanga, wakati zoezi la kuwapokea na kuwahifadhi raia hao wa Burundi likiendelea, juhudi mbalimbali zinaendelea za kuzungumza na serikali ya Burundi kwa ajili ya kuhakikisha kuwa utulivu unarejea nchini humo.
Nantanga amesema juhudi hizo zinazoratibiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, zinaongozwa na waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe ambaye anaongoza jopo la tume maalumu iliyoundwa na jumuiya hiyo kushughulikia mgogoro wa Burundi.
Aidha, Nantanga amesema raia hao wa Burundi bado hawajapata hadhi ya kuitwa wakimbizi na kwamba uwepo wao nchini utategemea zaidi hali ya usalama katika nchi yao.
Kwa sasa, msemaji huyo wa wizara ya mambo ya ndani ya nchi amewataka wananchi wanaoishi vijiji vya Tanzania vilivyo mpakani na Burundi, kutoa taarifa pindi wanapompokea mgeni yoyote ambaye si raia wa Tanzania na kwamba ni kosa kisheria kwa mtu yoyote kumhifadhi mgeni ambaye sio raia.