Alhamisi , 23rd Jul , 2015

Watu kumi wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria la Simiyu Express lililokuwa likitokea Bariadi kwenda Dar es salaam kupasuka tairi la mbele.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishina Msaidizi wa Polisi EMMANUEL G. LUKULA (ACP)

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma Emmanuel Lukula amesema ajali hiyo imehusisha gari lenye namba T 318 ABM lililopata ajali katika kijiji cha Chalinze Nyama Wilayani Chamwino mkoani Dodoma majira ya saa 12:30 jioni baada ya kupasuka tairi la mbele kushoto na kuacha njia na kuugonga mbuyu na kusababisha vifo vya watu 8 papohapo akiwemo na dereva wa basi hilo na majeruhi waliokimbizwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma.

Ezekiel Mpuya ni mganga mkuu wa mkoa wa Dodoma amethibitisha kupokea majeruhi 61 ambao kati yao 47 wamelazwa wakiwamo watoto watano na miili nane ya watu waliofariki katika eneo la tukio na watu wengine wawili walifariki wakati wakiendelea kupatiwa matibabu katika hospital ya rufaa ya mkoa wa Dodoma.

Ambao kati yao ni mwanamke mmoja aliyekuwa mjamzito na miili mingine tisa ni ya wanaume.

Dk Mpuya amesema baadhi ya majeruhi hali zao sio nzuri na jopo la madaktari linaendelea kuwapatia huduma katika hospitali hiyo.