Alhamisi , 8th Sep , 2022

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru ametangaza neema ya kuhamishwa wafanya biashara ndogondogo kutoka maeneo ambayo siyo rasmi na kuwapanga katika Soko la Wazi la Machinga kwa amani na utulivu ili waendelee kutekeleza majukumu yao.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru

Neema hiyo ameitangaza leo katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ambapo Mkurugenzi huyo aliongea na waandishi wa habari kuhusu kukamilika kwa Soko la Wazi la Machinga na kuwaeleza kuwa Machinga watahamishwa na kuingia sokoni kwa njia ya amani na hakuna vurugu yoyote itakayotokea.

Mkurugenzi Mafuru amesema “kuanzia leo tarehe 07/09/2022 mpaka tarehe 23/09/2022 wafanyabiashara wote niliowataja wanatakiwa wawepo ndani ya soko lile. Tumeshakubaliana Dodoma toka mwanzo kuwa hatapigwa mtu kirungu wala hatasukumwa mtu”.

Akizungumzia namna Jiji la Dodoma litakavyonufaika na ujenzi wa soko hilo, Mafuru alisema kuwa, kukamilika kwa Soko la wazi la Machinga kutasaidia jiji la Dodoma kuwa safi, na kutachangia mapato makubwa kwa Halmashauri.

“Huu mradi unakwenda kufanya mapinduzi kwa Jiji la Dodoma, cha kwanza tunachokwenda kukipata katika mradi huu, Jiji la Dodoma linakwenda kuwa safi katika kiwango hakijawahi kutokea tangu Dodoma kuumbwa. Tulichogundua na hata viongozi wa juu wamegundua hilo wafanyabiashara ndogondogo walifanya mji uonekane haupendezi pia soko hili litachangia mapato ya shilingi bilioni 1.2 ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mwaka” alisema Mafuru.