Jumanne , 10th Mei , 2022

Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imevunja rekodi kwa kupokea meli yenye magari 4397 ambayo yametoka nchini Japan na hivyo kuwa meli ambayo imepokelewa bandari ya Dar es salaam ikiwa na magari mengi zaidi. Awali, bandari ya Dar es salaam ilipokea meli yenye magari 4041 mwezi April 2022.

Sehemu ya magari 4397 yakiwa tayari yameshushwa bandarini

Mamlaka ya Bandari nchini Tanzania (TPA) imesema kuwa meli ya Meridian Ace ambayo imetia nanga katika bandari ya Dar es Salaam ikiwa na jumla ya magari 4397 kwasasa ndiyo meli ya kwanza kushusha magari mengi kwa pamoja katika historia ya bandari hiyo na TPA.

"Hii meli ya meridian ace imevunja rekodi kwa kuingiza magari 4397 kwa wakati mmoja, imevunja rekodi ya meli tuliyoipokea mwezi Aprili mwaka huu ambayo ilikuwa na magari 4041. Imetoka moja kwa moja nchini Japan lakini ilipita Singapore kabla ya kufika Tanzania"- Nicodemus Mushi, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano - TPA.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Mahusiano wa mamlaka ya bandari (TPA) Bw. Nicodemus Mushi amefafanua kwamba asilimia 23 ya magari hayo yanabakia nchini Tanzania huku asilimia 77 yakiwa ni ya mataifa nchi jirani. Ameongeza kuwa kupokea magari mengi kiasi hiki ni matokeo ya kuaminika kwa huduma za bandari ya Dar es salaam na kuwashukuru wadau kwa kuitumia bandari hiyo.

"Katika magari haya, 23% yanabakia nchini hapa na 77% ya magari haya yanakwenda nchi jirani ya Zambia, Malawi, Rwanda, Burundi, na Congo DR. Hii inamanisha kwamba wadau wetu wameendelea kuamini huduma za bandari ya Dar es salaam, lakini pia usalama, uharaka wa huduma na uaminifu" - Nicodemus Mushi, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano - TPA