Thursday , 30th Apr , 2015

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, imewekeza katika utafiti na kutenga zaidi ya shilingi bilioni 100 ili zifanikishe tafiti mbalimbali kwa maendeleo ya nchi.

Akizungumza jana wakati akizindua mtambo maalum wa kusafisha maji taka ya kiwanda cha kutengeneza mvinyo wa Banana, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia , Prof. Makame Mbarawa, amesema fedha hizo zimeanza kuzaa matunda kama uzinduzi huo ni moja ya matokeo ya utafiti huo.

Amesema kuwa fedha hizo zilitengwa mwaka 2010 na kati ya fedha hizo zimesaidia kusomesha watanzania zaidi ya 517 katika ngazi ya Uzamivu (PHD) na Uzamili (Masters).

Prof. Mbarawa amempongeza Profesa Kaloli Njau wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela kilichopo Arusha, kwa kuongoza timu ya utafiti ya Chuo Kikuu Dar es Salaam, SUA, Nelson Mandela na Makelele nchini Uganda na kuwezesha kugundua mtambo wa kusafisha maji taka ya viwandani na kuweza kuyatumia tena kwenye matumizi mengine.

Amesema kwa kutumia mtambo huo kiwanda kinaokoa fedha nyingi za kununulia mafuta, ambapo kabla ya mtambo huo kiwanda kilikuwa kinatumia lita zaidi ya 36,000 kwa mwaka, ila sasa wanatumia lita 100 pekee jambo ambalo la kupongezwa kwa kiwanda na watafiti.

Naye Prof. Kaloli Njau wa Chuo Kikuu cha Nelson Mandela na Mtafiti Mkuu wa Mradi wa kusafisha maji taka, amesema uvumbuzi wa mtambo huo ulianza tangu miaka ya 1995 Dar es Salaam, lengo kubwa likiwa kusaidia viwanda nchini kuokoa matumizi ya mafuta ya kuendeshea mitambo na kubana matumizi ya maji.

Amesema matokeo ya utafiti huo ni matunda ya watafiti watanzania, hali inayoonesha Tanzania ikijikita katika kuwekeza kwenye utafiti matunda yake yataonekana kwa haraka, sababu watu wapo na hatimaye nchi kupata sifa kubwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kiwanda cha Banana, Adolf Olomi, alishukuru kwa uzinduzi wa mtambo huo na kushukuru shirika la kiserikali lililo chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Sweden kwa kufadhili mradi huo kwa kutoa dola za Kimarekani 450,000.

Olomi amesema mbali na kusaidiwa lakini kama kiwanda waliwekeza zaidi ya shilingi milioni 404 na kufanya jumla ya fedha za kukamilisha mtambo huo hadi kufanya kazi ni zaidi ya shilingi bilioni moja zimetumika na mtambo unauwezo wa kutunza lita 200,000 za maji machafu, ila kwa sasa wanatunza lita 80,000.