Waziri Mkuu Tanzania na Mwenza wake wakiweka shada kwenye kaburi la mzee Mtei
Dkt. Mwigulu amemtaja kuwa kiongozi mahiri, mzalendo na nguzo muhimu katika historia ya uchumi na demokrasia ya Tanzania.
Akizungumza katika ibada hiyo ya mazishi iliyofanyika nyumbani kwa marehemu Tengeru, Dkt. Nchemba alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua mchango mkubwa wa marehemu kwa Taifa na Serikali mara zote itaenzi mchango wake mkubwa katika uchumi na demokrasia nchini.
Waziri Mkuu alisema Mzee Mtei alikuwa miongoni mwa Watanzania wachache waliobahatika kuhudumu katika nyadhifa zote kuu za sekta ya fedha, ikiwemo kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Waziri wa Fedha na mwakilishi wa Tanzania katika taasisi za fedha za kimataifa, mchango uliompa heshima ya kipekee kitaifa na kimataifa.
Alisema katika maisha yake ya utumishi wa umma, marehemu alitambulika kwa kusimamia misingi ya uadilifu, uaminifu, uzalendo, bidii na kumcha Mungu na kwamba mchango wake uliweka msingi imara wa taasisi za kifedha na nidhamu ya uchumi wa Taifa.
Dkt. Nchemba alibainisha kuwa Mzee Mtei pia alikuwa miongoni mwa waasisi wa demokrasia ya vyama vingi nchini, akiwa mwanzilishi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hatua iliyochangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mfumo wa kisiasa na uhuru wa mawazo nchini.
Katika kuenzi mchango wa marehemu kwa vitendo, Waziri Mkuu alitoa maelekezo mahsusi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa hatua hizo ni sehemu ya kudumisha misingi ya maendeleo, haki na uzalendo aliyoyaishi marehemu.
Waziri Mkuu alisisitiza kuwa utekelezaji wa maelekezo hayo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuendeleza maendeleo jumuishi, kusimamia haki za wananchi na kudumisha heshima ya viongozi waliolitumikia Taifa kwa uadilifu na uzalendo akiwemo Mzee wetu Mtei.








