
China imeapa leo Jumanne kwamba itapambana hadi mwisho dhidi ya ushuru wa asilimia 50 ambao Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kuiwekea nchi hiyo.
Hatua ambayo inaendelea kuzidisha vita vya kibiashara ambavyo tayari vimeanza kuyatikisa masoko ya kimataifa.
Hivi karibuni, China ambayo ni mpinzani mkuu wa kiuchumi wa Marekani ilitangaza mpango wa kuweka ushuru wa asilimia 34 kwa bidhaa za Marekani ambao unaanza kutekelezwa siku ya Alhamisi.
Hata hivyo, mpango huo wa China umejibiwa na Rais Trump ambaye amesema ikiwa China haitofuta ushuru wake wa asilimia 34 kwa bidhaa za Marekani basi itakabiliwa na ushuru mpya wa jumla ya asilimia 104.
Kwa upande mwingine, Mawaziri wa biashara wa Umoja wa Ulaya walikutana jana mjini Luxemburg kujadili namna watakavyopambana na ushuru mpya uliotangazawa na Marekani kwa bidhaa kutoka Ulaya.