Monday , 11th Sep , 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amewaomba viongozi mbalimbali nchini wakiwemo wa dini, siasa na kimila pamoja na wazazi kuhakikisha suala la maadili kwa vijana linaimarika ili kuepusha kuwa na Taifa la vijana wasiozingatia maadili.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan,

Kauli hiyo ameitoa hii leo Septemba 11, 2023, jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano maalum wa Baraza la Viongozi wa Vyama vya Siasa na wadau wa demokrasia, na kusisitiza kwamba kwa yale yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii watu kutukana hovyo itakuwa ni vigumu kupata viongozi wenye maadili hapo baadaye.

"Mmomonyoko wa maadili tunaozungumza hapa, hawa ndiyo sasa wanakuja sijui wanafanya kitu gani huko anapata pesa yake anakwenda anapiga kampeni anaingia kwenye chama, anapitia kwenye chama kwa sababu viongozi huku juu tuko wanaopitia kwenye chama na waliotokana na vyama, waliotokana na vyama wamesimama vizuri waliopitia kwenye vyama ndiyo wanaotuhangaisha," amesema Rais Samia

Aidha Rais Samia ameongeza kuwa, "hakuna uungwana lipo tu, mimi huwa najiuliza hivi ule mdomo unaopukutisha matusi ni uleule anaotumia kula chakula ukampa siha ya mwili wake, huwa najiuliza huyu mtu ana midomo miwili wa matusi na wa kula?, au mdomo ule ndiyo anaokaa na mke wake akazungumza ya maana kweli, wakapanga nakupenda, nakupenda darling mdomo ule ule kweli au wana midomo mingapi wenzetu,".