Mkurugenzi wa Kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Bi Adelaide Salema
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya filamu ya Mwanahiti inayohusiana na kutunza mila na utamaduni wa mtoto wa kike wakati wa kuvunja ungo, Mkurugenzi wa Kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Bi Adelaide Salema amesema filamu hiyo imekuja wakati muafaka kwa kuwa itawezesha jamii ya watanzania hususan vijana kuepukana na athari zinazotokana na uelewa mdogo wa mila na tamaduni za kitanzania.
Salema licha ya kuupongeza uongozi wa Jukwaa la Picha Time na Balcony Series kwa kukabidhi filamu hiyo Makumbusho ya Taifa la Tanzania, ametoa wito kwa wadau wengine kushirikiana na Kituo Cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni katika kuhifadhi na kurithisha jamii urithi adhimu wa utamaduni uliopo nchini.
Wakikabidhi filamu hiyo, watengenezaji wa makala hiyo ya kiutamaduni, Haikaeli Gilliard wa jukwaa la balcony series na Nicholas Mwakatobe kutoka jukwaa la picha time wamesema wameona vyema washirikiane na serikali katika kuhifadhi urithi huo wa kitamaduni ili uweze kutumika katika kutoa elimu kwa wanaotembelea Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni.
Mwanahiti, ni kinyago maalum kinachotumiwa na makabila ya watu wa Pwani kufundishia mabinti wanaoingia hatua ya utu uzima ili kujenga jamii inayotambua wajibu wake kwa faida ya jamii husika.