Saturday , 19th Nov , 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa siku saba kwa Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha wanatatua changamoto inayokwamisha ujenzi wa barabara ya Pangani - Makurunge Bagamoyo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango

Barabara hiyo imekwama kutokana na eneo la jiwe la kuchimba kokoto leseni yake ya uchimbaji kupewa mtu mwingine tofauti na mkandarasi husika.

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 19 Novemba 2022 wakati aliposimama kuzungumza na wananchi wa Mkata Wilaya ya Handeni mkoani Tanga akiwa njiani kuelekea makao makuu ya mkoa huo kwaajili ya ziara.

Ameagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuhakikisha wanafanyia kazi mapema zaidi maeneo yanayotumika kwaajili ya ujenzi wanayoyapata baada ya tafiti wanazofanya ili kuepusha migogoro inayokwamisha maendeleo ya miradi.

Pia ameagiza kutatuliwa mara moja changamoto iliokwamisha ujenzi wa barabara ya Handeni - Kibirashi – Kiteto hadi Dodoma ambayo ujenzi wake ulipaswa kuanza tangu mwezi Mei mwaka huu.

Aidha Makamu wa Rais ameagiza uongozi wa mkoa wa Tanga kuhakikisha wanafanya vikao na wafugaji kwa lengo la kuwapa elimu ya sheria na taratibu za nchi ili kuondokana na migogoro inasababishwa na wafugaji kulisha mifugo katika mashamba ya wakulima. 

Pia Makamu wa Rais ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama wilayani Handeni kufuatilia na kuwachukulia hatua wafugaji waliowajeruhi wakulima wakiwa mashambani ili kulinda amani iliopo nchini.