Saturday , 24th Sep , 2022

Kamati ya kushughulikia migogoro ya ardhi iliyoundwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi itaendelea kutatua changamoto za ardhi katika mkoa wa Dodoma kuanzia siku ya jumatatu tarehe 26 hadi 30 Sept 2022.

Awali kamati hiyo ilisikiliza na kutatua changamoto za ardhi katika mkoa wa Dar es Salaam ambapo zaidi ya changamoto 150 za migogoro ya ardhi zilipatiwa ufumbuzi.

 

Maeneo ambayo kamati hiyo itasikiliza na kutatua changamoto za migogoro ya ardhi katika mkoa wa Dodoma ni Mkonze, Kikuyu Kaskazini na Kusini, Ipagala na Makole, Makulu na Iyumbu pamoja na maeneo ya Nzuguni, Mtumba na Kikombo.

 

Katibu Mkuu wa wizara ya Ardhi Dkt Allan Kijazi alisema, lengo la kuanzisha utaratibu huo wa kutatua changamoto za ardhi ni kupunguza migogoro ya ardhi inayolalamikiwa.

 

Hata hivyo, alisema kuwa, kamati hiyo itakayohusisha taasisi mbalimbali vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama haitashughulika na migogoro ya ardhi ambayo kesi zake ziko mahakamani.

 

Kwa mujibu wa Dkt Kijazi, uzoefu unaonesha migogoro mingi ya ardhi inasababishwa na uelewa mdogo wa sheria pamoja na taratibu mbalimbali za umiliki jambo alilolieleza kuwa linasababisha wajanja wachache kutumia udhaifu huo kuwalaghai au kudhulukmu wananchi.