Zao la Pamba likiwa kwenye Maghala.
Wakulima hao wameyasema hayo wakati wakipokea mbegu bora za Alizeti kilo 1800, walizopewa kama msaada za kutoka kampuni ya kichina ya Jielong Holdings (LTD), iliyopo mjini Shinyanga.
Wamesema, zao hilo la pamba ambalo kwa miaka ya nyuma lilikuwa mkombozi kwa wakulima wengi, lakini miaka ya hivi karibuni limekuwa likiwatia hasara, na kuwarudisha nyuma kimaendeleo, ambapo hivi sasa wameamua kuachana nalo na kujikita zaidi katika zao la Alizeti.
Naye afisa utawala wa kampuni hiyo ya kichina Athanas Wiliamu, amesema wameamua kutoa msaada wa mbengu hizo za Alizeti katika kijiji cha jirani na kampuni hiyo, ili kuwapunguzia gharama za kilimo pamoja na kuwahamasisha kulima zao hilo ambalo litawakomboa kimaisha.
Amesema, kwa sasa kampuni hiyo inalazimika kununua Alzeti kutoka mikoa yote hapa nchini, ambayo inalima zao hilo, badala ya kutegemea malighafi hiyo kutoka nje ya nchi na kukamua mafuta, kwa lengo la kuinua uchumi wa watanzania na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake afisa kilimo wa halmashauri ya Shinyanga vijijini Oscar Jeremia, amesema endapo wakulima wakihamasishwa kulima kilimo cha Alizeti kwa wingi, itasaidia kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri hiyo kupitia kilimo, pamoja na kukuza pato la mtu mmoja mmoja, hali ambayo itaondoa janga la umaskini kwa wakulima.
Jeremia ameongeza kuwa, asilimia kubwa ya wakulima wamekuwa wakulima kila mwaka, lakini hawapati mafanikio kutokana na kulima mazao ambayo hayana faida, wala masoko ya uhakika, huku yakiwatia hasara na kuwasababishia kuendelea kuwa masikini kutokana na kutojua mazao gani mbadala ya kulima ambayo yatawakwamua kiuchumi.