Naibu waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia mheshimiwa Januari Makamba ambaye ametangaza nia ya kugombea nafasi ya urais, amewaomba viongozi wa dini nchini kuliombea taifa katika uchaguzi mkuu ujao wa Rais na Wabunge ili watanzania waweze kumchagua Rais mwenye hekima, busara na kutenda haki kwa wote.
Mheshimiwa makamba ametoa ombi hilo wakati akizungumza na viongozi wa kanisa Anglikana Dayosisi ya Tanga wakati wa jubilee ya kanisa la mtakatifu Luka lililojengwa na wamisionari baada ya kutimiza miaka 125 tangu kujengwa kwake iliyofanyika katika kanisa hilo lililopo kata ya misozwe wilayani muheza.
Katika sherehe hizo Askofu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Tanga Dkt. William Mndolwa amewataka waumini na wakazi wa mkoa wa Tanga kujitolea damu kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wenye mahitaji ya damu hasa majeruhi wa ajali mbalimbali zikiwemo za barabarani pamoja na akina mama wajawazito wanaofikishwa katika hospitali teule ya wilaya ya mtakatifu Augustino Muheza kufuatia makundi hayo kuhangaikia huduma ya damu inayosababisha baadhi yao kupoteza maisha kwa sababu ya ukosefu wa huduma hiyo.
Katika sherehe hizo jumla ya shilingi milioni 13 zilichangwa na waumini pamoja na wageni waalikwa kwa ajili ya ukarabati wa Kanisa la Mtakatifu Luka lililojengwa miaka 127 iliyopita pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa ya shule ya awali ili kukuza elimu kuanzia ngazi za vijiji, kata hadi taifa.