Friday , 3rd Jan , 2020

Kiungo pendwa nchini Tanzania, Haruna Niyonzima amewasili nchini Januari 2 tayari kuanza majukumu ya kuitumikia klabu ya Yanga baada ya kumalizana wiki iliyopita.

Haruna Niyonzima baada ya kuwasili nchini

Niyonzima alipokelewa na Afisa Mhamasishaji na Msemaji wa klabu hiyo, Antonio Nugaz majira ya mchana na moja kwa moja akajiunga kambini, kujiandaa na mchezo mkubwa dhidi ya mahasimu wao Simba utakaopigwa kesho Januari 4, 2020.

Swali lililopo kwa mashabiki wengi wa klabu ya Yanga ni iwapo Haruna atacheza katika mchezo huo ama la! kutokana na kutofanya mazoezi na timu kwa kipindi kirefu, lakini mwenyewe amesema kuwa yuko fiti kucheza mchezo huo.

"Nipo tayari hata kwa mchezo dhidi ya Simba SC japo sipendi kuongelea sana kwa maana mechi hizi zina mambo mengi sana lakini kikubwa ni kujiandaa kisaikolojia. Narudi nyumbani Yanga", amesema Niyonzima mara baaya ya kuwasili nchini.

Timu hizi zinakutana zikiwa na rekodi nzuri katika michezo yao mitatu iliyopita, Yanga ikitoka sare ya bila kufungana na Mbeya City, ikipata ushindi dhidi ya Tanzania Prisons na ushindi wa mwisho dhidi ya Biashara United huku Simba ikishinda michezo yake mitatu dhidi ya Ndanda FC, KMC na Lipuli FC.