Monday , 30th Dec , 2019

Wazazi wa watoto 24 wanaodaiwa kulawitiwa na mwanaume mmoja,aliyejulikana kwa jina la Arnold Mlay, mkazi wa Semtema A, Manispaa ya Iringa, mkoani humo, wamesema mtuhumiwa huyo alikuwa akiwarubuni watoto kwa zawadi ndogo ndogo na kuwatishia kuwaua kwa yeyote atakayetoa taarifa kwa Mzazi.

Hayo yamebainishwa leo Disemba 30, 2019, na Evelina Magova na Grace Kivilo, ambao ni wazazi wa watoto waliokumbwa na mkasa huo, katika mkutano wa dharula ulioitishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Richard Kasesela, ambapo wamesema kuwa Mlay ana kituo cha kuchezesha michezo ya watoto 'Games' ambapo kwa nyakati tofauti alitumia nafasi hiyo, kuwafanyia ukatili watoto wao.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo Richard Kasesela, ameshtushwa na ukubwa wa tatizo hilo na kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuunda kamati ya watu 10, ili kuendelea kubaini watoto ambao wamefanyiwa ukatili wakijinsia.

Mtuhumiwa wa ukatili huo kwa watoto mkoani humo, anaendelea kushikiliwa na jeshi la Polisi na upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani .