Thursday , 24th Oct , 2019

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo, ameiagiza Wizara yake kuhakikisha wataalam wa Sekta ya maendeleo ya jamii, wanapewa jukumu la kusimamia kazi  ya  Bima ya Afya ya Jamii (CHF), iliyoboreshwa katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri kwa kuwa ndiyo

wenye utaalam wa kuhamasisha jamii.

Waziri Jafo ameyasema hayo wakati wa kufunga Kongamano la Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wataalam wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii, lililofanyika jijini Dodoma kwa siku tatu na kuwataka wataalam hao, kutumia taaluma yao ipasavyo kufanikisha zoezi hilo.

Aidha Waziri Jafo ameongeza kuwa, kazi hiyo imekuwa ikitekelezwa na wataalam wa sekta ya Afya, ambao kitaaluma wanafani ya tiba na madawa, lakini linapokuja suala la uhamasishaji wa jamii kuhamasisha kushiriki masuala ya maendeleo ni wataalam wa maendeleo ya jamii waliobobea katika fani hiyo.

Katika wafanyakazi ambao wamekuwa hawapewi kipaumbele na kudhalauliwa katika maeneo yao ya kazi ni wataalam wa maendeleo ya jamii lakini sasa wakati umefika kuwapatia vitendea kazi na kuwatumia katika shughuli zote za maendeleo ya Taifa”. Aliongeza Waziri Jaffo.

Aidha Waziri Jafo ameongeza kuwa kwa kipindi kirefu wataalam hawa, wamekuwa hawatumiki ipasavyo na badala yake wamekuwa wakitumiwa wakati wa dharula au katika kazi za zimamoto.

Waziri Jafo pia amewataka wataalam hao wa maendeleo ya jamii, kujiamini katika utendaji kazi wao na kuhakikisha wanasimamia misimamo katika vikao vya mbalimbali vya maamuzi, ikiwemo CMT ili waweze kukubalika na kuaminika kama ilivyo kada nyingine katika maeneo yao ya kazi.