Friday , 6th May , 2016

Watanzania wametakiwa kuwapa elimu watoto mwenye ulemavu na kuachana na dhana ya kuwa walemavu hawawezi, kwani wakipatiwa elimu wanaweza kujitegemea kama watoto wengine .

Watoto wenye Mahitaji Maalum wakiwa darasani

Wakiongea na East Africa Radio, baadhi watu wenye ulemavu mkoa wa Arusha wamesema kwa kipindi kirefu jamii imekuwa ikiwatenga hasa katika upatikanaji wa elimu,jambo ambalo limekuwa likisababisha baadhi yao kuwa ombaomba.

Dyness Godfrey ni miongoni mwa watumiaji wa vifaa tiba ambapo ameeleza kuwa vifaa hivyo ni ghali, jambo ambalo wengi wao wanashindwa kupata hivyo kukosa mahitaji yao ya kila siku.

Nae Mwenyekiti wa Chama cha Wenye Ulemavu mkoa wa Arusha amesema pamoja na kuwa na changamoto nyingi kwa sasa wametoa mapendekezo yao kwa serikali ,ambayo wanaamini iwapo yatawasilishwa bungeni na kupitishwa changamoto hizo zitatatuliwa.

Afisa Maendeleo ya jamii kutoka shirika la Hims Maclini Rumanyika, amesema kazi iliopo kwa sasa ni serikali kuendelea kutoa elimu kwa jamii na kusimamia kwa umakini sera ya walemavu,ili kuhakikisha walemavu wanapata mahitaji muhimu kama watu wengine.

Ameongeza kuwa ikiwa serikali ina nia ya makusudi ya kuondoa ombaomba katika maeneo ya mijini, umefika wakati kuhakikisha kila mwenye ulemavu anapatiwa elimu na stadi za maisha ili aweze kujitegemea.