Monday , 22nd Feb , 2016

Serikali mkoani Kilimanjaro imerejesha mashamba yenye ukubwa wa hekari 2470 kwa wananchi wa vijiji viwili vya Lotima na Makuyuni wilaya ya Moshi ambayo yalichukuliwa kwa makosa kwa lengo la kujenga soko la kimataifa la mazao ya nafaka eneo Himo.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makala

Mashamba hayo ambayo awali yalichukuliwa na serikali ya mkoa kinyume cha sheria yamerejeshwa kwenye chama cha ushirika cha kilimo, mifugo na uzalishaji mali (Lokolova) na mkuu wa mkoa wa kilimanjaro Bw. Amos Makala baada ya kukiri kuwa serikali ilichukua mashamba hayo kwa makosa.

Amesema awali serikali ilipewa hekari 140 za kujenga soko hilo la nafaka lakini baadaye serikali ilitaifisha mashamba hayo yenye ukubwa wa hekari 2470 bila makubaliano na wananchi hali iliyoibua mgogoro wa muda mrefu baina ya wananchi na serikali.

Baadhi ya wananchi na wanachama wa chama cha ushirika cha Lokolova wamesema kwa zaidi ya mika mitano wamekuwa wakiteseka baada ya mashamba yao kutaifishwa na kufuta chama cha ushirika hali iliyowakwamisha kuendeleza shughuli za kilimio na ufugaji.