Tuesday , 29th Sep , 2015

Msanii wa Hip Hop kutoka Bongo Roma Mkatoliki, amesema yeye hana taarifa rasmi za kufungiwa kwa wimbo wake aliouchia hivi karibuni wa Viva roma, ambao umeleta utata mkubwa kwa jamii kutokana na mashairi yake.

Roma amefunguka kuhusu sakata hilo kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na east Africa Radio, na kueleza kwamba nae amepata taarifa hiyo kupitia kwenye moja ya chombo cha habari kuandika kuhusu taarifa hiyo.

"Sina jibu la moja kwa moja na napata kigugumizi kwa sababu sina taarifa rasmi kwa kweli, yani finaly mimi nakuwa kama shabiki tu tena, vile shabiki alivyoona ndivyo mimi kama Roma nilivyoona, niliamka tu na mimi nikaona kama kuna chombo kimoja cha habari kimepost katika akaunti ya Instagram, kwamba kuna tamko limetoka BASATA kwamba limefungia nyimbo ya Roma, kwa sababu ambazo walizianisha", alisema Roma.

Pia Roma aliendelea kwa kusema kwamba chombo kinachosimamia sanaa hajui wanatumia njia zipi ili kufikisha taarifa zao kwa jamii.

"Nisiwe muongo sijui taratibu kinakuwa kinatumia kufikisha information zao, kwa sababu kitu ambacho naona ingekuwa rahisi kama artist kabla hajaachia nyimbo yake mpya ama hajafanya kazi yake ya sanaa, iwe inawasilishwa katika hiko chombo, nadhani hapo tungekuwa tunaenda sawa.

Timu ya Planet Bongo iliamua kumtafuta Afisa Habari wa BASATA Bwana .Aristide Kwizela, na kusema kwamba sio lazima kwa wao kutoa barua rasmi kwa msanii, ila wanaweza wakatoa taarifa kwa uma.

"Kuna kufungia kwa maana ya msanii mwenyewe kuandikiwa, lakini kama kuna taarifa imetoka public kwamba nyimbo za namna hiyo zimezuiliwa, kuna two way either barua kuandikwa kwa msanii au pia kuna public anouncements kwamba wimbo fulani umefungiwa", alisema Bwn. Kwizela.