Sunday , 9th Aug , 2015

Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF limesema halitaruhusu viwanja vilivyo chini ya viwango vya ubora unaotakiwa kwaajili ya kuchezezwa ligi za soka hapa nchini vitumike kama havijafanyiwa marekebisho kufikia ubora unaotakiwa na shirikisho hilo.

Jengo la ofisi ya makao makuu ya shirikisho la soka nchini Tanzania TFF maeneo ya Karume jijini Dar es Salaam.

Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limewataka wamiliki wa viwanja ambavyo vitatumika kwa ngalambe za michuano ya Ligi Kuu (VPL), Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL) ambazo zitaanza mwezi ujao wahakikishe wanakamilisha marekebisho ya mapungufu ya viwanja vyao mapema.

Afisa habari wa TFF Baraka Kizuguto amesema hatua hiyo ni agizo la wakaguzi ambao walienda kuvikagua viwanja husika ambavyo vitatumika kwa ligi hizo na kimsingi TFF inaamini wahusika watafanyia kazi mapungufu hayo haraka iwezekanavyo kabla ya ligi hizo kuanza.

Aidha Kizuguto amesema kila kiwanja kina mapungufu ya tofauti japo vichache vinalingana mapungufu yake ila vingine vinamapungufu makubwa kitu ambacho kinahitaji nguvu ya ziada kuhakikisha wanafanya marekebisho ya haraka hasa ikizingatiwa wamepata fursa ya kuongezwa kwa muda wa kuanza kwa ligi kuu basi nao ni vema wakatumia muda huo wa nyongeza kukamilisha ukarabati huo mapema iwezekanavyo.

Kwaupande mwingine shirikisho la soka nchini Tanzania TFF limesema ni viwanja vinne pekee ndivyo mpaka sasa vimepitishwa kwakuwa na vigezo vyote vya viwango vya ubora wakuchezewa ligi mbalimbali zinazosimamiwa na shirikisho hilo hapa nchini.

Viwanja hivyo vinne ambavyo vimepitishwa na shirikisho hilo vyote viko jijini Dar es Salaam na kimoja kule mwanza ambavyo ni Uwanaj wa Taifa, Uwanja wa Karume na Azam Complex Chamazi vyote vya Dar es Salaam an ule wa CCM Kilumba jijini Mwanza.