Sunday , 3rd May , 2015

Ukisikia usemi wa ng'ombe wa masikini hazai unaweza ukakubali hii ni baada ya soka la Tanzania kushuhudia timu pekee iliyosalia katika michuano ya vilabu barani Afrika Yanga nayo ikiaga michuano hiyo baada ya kufungwa bao 1-0 na Etoile du Sahel

Baadhi ya wachezaji wa Yanga wakishangilia goli katika moja ya michezo yao.

Wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Yanga wametolewa baada ya kufungwa kwa bao 1-0 dhidi ya Etoile du Sahel.

Mechi hiyo ya pili ya kombe la shirikisho kwenye uwanja wa Olimpiki mjini Sousse, Tunisia, imeifanya Yanga ing’oke kwa jumla ya mabao 2-1 ikiwa ni baada ya sare ya bao 1-1 jijini Dar.

Yanga ilionyesha mchezo mzuri lakini bao la kipindi cha kwanza lililofungwa na nahodha Amar Jemal kwa kichwa, ndiyo lililowang’oa.

Kipindi cha pili, bado Yanga ilionyesha soka safi lakini ilipoteza nafasi kadhaa.

Mshambuliaji wake, Amissi Tambwe alionekana kuwa msumbufu kwa mabeki wa Etoile. Lakini mwisho mechi hiyo imeisha kwa wawakilishi hao wa Tanzania kung’olewa.

Ambapo baada ya matokeo hayo mashabiki na wanachama wa timu hiyo wametaka utulivu ndani ya klabu hiyo wakati huu ikijiandaa kumalizia mechi mbili za ligi kuu Tanzania bara dhidi ya Azam FC Jumatano wiki ijayo na ule dhidi ya Ndanda mwishoni mwa ligi hiyo.

Hivyo wanachama na mashabiki hao wameutaka uongozi wao kujipanga upya badala ya kuanza kutafuta mchawi.

Wakiongea na muhtasari wa michezo baadhi ya wanachama wa klabu hiyo wamesema ni fursa sasa ya uongozi kumpa nafasi mwalimu ama kocha mkuu wa timu hiyo kwakushirikiana na benchi la ufundi ili afanye usajili yeye mwenyewe na aiboreshe timu kwani kwa muda mfupi aliokuwa na timu hiyo ameweza kuibadilisha na kuipa makali na uwezo wa kucheza na timu yoyote hapa duniani wakitolea mfano hata Barcelona ya uhispania.

Aidha wanachama hao wamesema kwa kiwango kilichooneshwa jana na timu hiyo hakuna ambaye atapinga juu ya uwezo mzuri wa kocha huyo japo kuna mapungufu machache ambayo pengine akipata muda mrefu zaidi wa kukaa na kikosi hicho na kukiunda upya anaweza kuyamaliza na kikosi hicho kikafanya vema msimu ujao kwakuwa wao ni mabingwa hivyo watashiriki klabu bingwa barani Afrika kwa mara nyingine.