Kocha wa Yanga Hans van der Pluijm (kulia) na Msaidizi wake Juma Mwambusi wakiteta jambo.
Mwambusi amesema hayo wakati wa mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na ameshukuru kikosi kukamilika kwa wachezaji wote kufika mazoezini.
Yanga ambao ni wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika CAF CC wanataraji kukutana na Mouloudia Olympique Bejaia wiki ijayo mwishoni kati ya tarehe 16 hadi 19 Juni mwaka huu.
Mwambusi amesema wamewaandaa wachezaji hao kisaikolojia kuhakikisha wanakabiliana na figisu na hila zote za waarabu hao na kimsingi wako tayari kwakuwa tayari wanauzoefu wa kutosha kuhimili mbinu zote chafu za Waarabu kwakuwa tayari walishapitia changamoto hiyo dhidi ya Al Ahly ya Misri na kubwa zaidi hila za wazi walizokutana nazo nchini Angola walipokwenda kurudiana na Sagrada Esperanca.
Akimalizia Mwambusi amesema anajua mchezo huo utakuwa mgumu zaidi kutokana na mazingira na ubora wa wapinzani ambapo pia wamejipanga kucheza kwa tahadhali kubwa hasa ikizingatiwa mchezo huo unachezeshwa na waamuzi kutoka Morocco nchi ya Waarabu wengine wa Afrika.
Kwaupande wake Daktari wa timu hiyo Edward Bovu akizungumzia afya na utimamu wa mwili kwa wachezaji wa timu hiyo amesema ameridhika na hali ya wachezaji wake wako timamu na pia hakuna majerui mkubwa ambaye pengine akakosa mchezo huo.
Wakati huo huo waamzui kutoka nchini Morocco wameteuliwa kuchezesha mechi ya ufunguzi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, kati ya wenyeji Mouloudia Olympique Bejaia na Yanga SC ya Tanzania Juni 19, mwaka huu.
Mchezo huo wa Kundi A utafanyika Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia, Algeria utachezeshwa na Bouchaib El Ahrach atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera, Redouane Achik na Youssef Mabrouk.
Baada ya mchezo huo, Yanga itarejea Dar es Salaam kuwakaribisha mabingwa wa Afrika, TP Mazembe Juni 28 katika mchezo wake wa pili wa Kundi A.
Kwa sasa ni kiungo mshambuliaji mwenye kasi ya ajabu Simon Msuva ndiye pekee anaendelea na dozi ya malaria na kabla ya kufika mchezo huo basi atakuwa tayari kurejea dimbani kuitumikia timu hiyo.
Na katika mchezo huo, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limechanganya marefa kutoka nchi tatu tofauti, ambao ni Janny Sikazwe wa Zambia atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Jerson Emiliano Dos Santos wa Angola na Berhe O'michael wa Eritrea.
Timu nyingine katika Kundi A ni Medeama ya Ghana ambayo itafungua dimba na TP Mazembe mjini Lubumbashi Juni 17, mwaka huu, mchezo ambao utachezeshwa na marefa wa Shelisheli Bernard Camille, Hensley Danny Petrousse na Eldrick Adelaide.