Saturday , 16th Apr , 2016

Yanga imekamilisha vema safari yake ya kula viporo vitatu vya michezo ya Ligi Kuu Tanzania bara baada ya leo kukamilisha kula kiporo cha tatu dhidi ya Mtibwa Sugar na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo mkali uliopigwa katika uwanja wa Taifa.

Kikosi cha timu ya soka ya Yanga.

Mabingwa wa tetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania bara timu ya Yanga SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara VPL baada ya ushindi wa bao 1-0 jioni ya leo dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro, katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Shukrani kwake, mfungaji wa bao hilo pekee, Simon Happygod Msuva akifunga goli hilo mwanzo wa kipindi cha pili dakika ya 47 kwa shuti la umbali wa mita 28 baada ya kuanzishiwa mpira wa adhabu ndogo na kiungo Haruna Niyonzima.

Sasa Yanga SC inafikisha pointi 59 baada ya kucheza mechi 24 na kuwashusha waliokuwa vinara wa ligi hiyo kwa muda mrefu timu ya Simba SC hadi nafasi ya pili wakiwa na pointi 57 kwa mechi 24.

Hata hivyo Yanga ambao kesho wanataraji kusafiri kuelekea nchini Misri kwa mchezo wa marudiano wa kuwania Klabu Bingwa barani Afrika dhidi ya Al Ahly ya huko mchezo utakaopigwa Aprili 20,na huenda watakaa kileleni kwa saa 24 pekee kwani mahasimu wao Simba SC wanaweza kurejea kileleni kesho wakiifunga Toto Africans kwenye Uwanja huo huo katika mchezo mwingine wa ligi hiyo.

Katika kipindi cha kwanza, kocha Mholanzi wa Yanga, Hans van der Pluijm alianzisha mabeki watatu wa kati kwa pamoja, Kevin Yondan, Vincent Bossou na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, huku akitumia mshambuliaji mmoja, Donald Ngoma.

Hali hiyo iliwafanya Yanga wasiwe na makali sana katika safu yao ya ushambuliaji, huku krosi nyingi za kutokea pembeni zikipitiliza au kuchezwa na mabeki wa Mtibwa Sugar.

Lakini mabadiliko aliyoyafanya Pluijm anayesaidiwa na mzalendo, Juma Mwambusi mapema kipindi cha pili kumtoa beki mmoja wa kati, Yondan na kumuingiza mshambuliaji, Malimi Busungu yalirudisha makali ya safu ya ushambuliaji ya Yanga.

Hata hivyo, safu ya ulinzi ya Mtibwa Sugar ikiongozwa na kipa wa zamani wa Yanga, Said Mohammed iliendelea kuwa imara na kutoruhusu mabao zaidi.

Katika michezo mingine ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara Coastal Union imeifunga JKT Ruvu bao 1-0 huku Ndanda FC ikiichapa Kagera Sugar mabao 2-0.