Kikosi cha timu ya soka ya Simba.
Ikicheza mchezo wa nne mfululizo na watatu wa ligi kuu ikiwa chini ya kocha wa muda Mganda Jackson Mayanja katika dimba la Taifa,jijini Dar es salaam wekundu wa Msimbazi, Simba SC wameitandika ama kuisulubu timu ya wana kimanumanu African Sports ya Tanga kwa jumla ya mabao 4-0.
Ushindi huo muhimu, unaifanya Simba SC ifikishe pointi 36 baada ya kucheza mechi 16, sasa ikizidiwa pointi tatu na vinara, Yanga na Azam FC wenye pointi 39 kila mmoja.
Simba ilianza kuhesabu karamu hiyo ya magoli kupitia bao la kwanza la dakika ya 14 lililofungwa na mshambuliaji Mganda, Hamisi Kiiza aliyefumua shuti kali kwa mguu wa kushoto baada ya pasi nzuri toka wingi ya kulia iliyopigwa na beki mwenye kasi ya ajabu kinda Hassan Kessy.
Kessy mwenyewe akafunga goli la pili kunako dakika ya 30 kwa shuti la mguu wa kulia akimalizia pasi ya mshambuliaji Ibrahim Hajib na kabla ya kufunga bao hilo aliwachambu mabeki na pia kumchambua vizuri kipa Zakaria Mwaluko.
Kiiza tena ambaye leo alicheza kwa ustadi mkubwa alifanikiwa kumlamba chenga kipa Mwaluko baada ya kupata pasi ya kiungo Mwinyi Kazimoto na kuifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 42.
Karamu ya magoli ya Simba ilihitimishwa na kinda mwenye kipaji cha hali ya juu Hajji Ugando baada ya kuifungia Simba SC bao la nne dakika ya 75 akipokea pasi nzuri ya kiungo aliyekuwa katika kiwango kizuri siku ya leo Jonas Mkude.
Kwa upande wao mahasimu wa Simba na vinara wa ligi kuu Tanzania bara Yanga SC wamejikuta wakiduwazwa na wenyeji wao wagosi wa kaya baada ya kukubali kichapo kizito cha bao 2-0 mbele ya Coastal Union mchezo ukichukua nafasi katika dimba la Mkwakwani, jijini Tanga.
Matokeo hayo yanawafanya wanajangwani hao wabaki na pointi zao 39 baada ya kucheza mechi 16, sawa na Azam FC iliyocheza mechi 15 baada ya mchezo wao dhidi ya maafande wa Magereza toka Mbeya kusogezwa mbele kutokana na mabingwa hao wa kombe la Kagame kuwa katika ziara nchini Zambia.
Coastal Union waliocheza kiwango bora siku ya leo walipata bao lao la kwanza dakika ya 27 kupitia kwa beki wa zamani wa Simba SC, Miraj Adam aliyefunga kwa shuti la mpira wa adhabu lililomparaza mikononi kipa Deo Munishi ‘Dida’ kabla ya kutinga nyavuni kupitia katikati ya miguu.
Refa Andrew Shamba wa Pwani aliwapa nafasi ya kupiga faulo Coastal Union, baada Miraj Adam mwenyewe kuangushwa na beki wa Yanga, Kelvin Yondan nje kidogo ya boksi.
Ushindi Mujarabu wa Coastal Union ulihitimishwa na mshambuliaji chipukizi, Juma Mahadhi aliyefunga bao la pili kwa timu hiyo dakika ya 62 baada ya pasi nzuri ya Hamad Juma nakufanya hicho kiwe kipigo cha kwanza kwa vinara hao wa ligi kuu Tanzania bara na hivyo kuiacha Azam FC kusalia kuwa ndiyo timu pekee ambayo bado haijaonja chungu ya kufungwa katika ligi hiyo ambayo hii leo ndiyo imeingia mzunguko wa pili .
Bao hilo liliwavunja nguvu kabisa wachezaji wa Yanga SC na kujikuta wanacheza bila malengo. Refa Andrew Shamba alimtoa kwa kadi nyekundu beki wa Yanga, Kevin Yondan dakika ya 100. baada ya awali, dakika ya 97 Shamba alijichanganya kwa kumuonesha kadi nyekundu Said Jeilan badala ya njano.
Matokeo mengine ya michezo iliyochezwa hii leo ni maafande wa JKT Ruvu wametoshana nguvu baada ya kwenda sare tasa ya 0-0 na Majimaji katika mchezo mkali uliopigwa katika uwanja wa kumbukumbu ya Karume jijini Dar es salaam.
Mchezo mwingine ulikuwa huko Shinyaka katika dimba la Mwadui Complex wakati wenyeji Mwadui FC wakiwachapa kwa bao 1-0 wana kishamapanda timu ya Toto Africans ya Mwanza.
Ligi hiyo itaendelea Jumapili hii Januari 31 kwa mitanange miwili kupigwa ambapo katika dimba la Mkwakwani jijini Tanga wenyeji maafande wa Mgambo JKT watawaalika wamachinga toka Mtwara timu ya soka ya Ndanda FC.
Mtibwa Sugar Vs Stand United