Sunday , 1st Mar , 2015

Azam Fc imeaga mashindano ya Ligi ya mabingwa Afrika baada ya kufungwa mabao 3-0 katika mchezo wa marudiano wa mzunguko wa awali uliofanyika Uwanja wa Marreikh mjini Khartoum.

Pamoja na kupewa Penati ambayo iliokolewa na kipa Aishi Manula, Merreikh ilimaliza dakika 45 za kwanza ikiwa inaongoza bao 1-0 katika mchezo huo uliochezeshwa na waamuzi kutoka Zambia Wellington Kaoma aliyesaidiwa na Romeo Kasengele na Amos Nanga.

Kipindi cha pili Merreikh ikafanikiwa kushinda mabao mawili zaidi yaliyofungwa na Ahmed Abdallah dakika ya 85 na Allan Wanga dakika ya 90.

Azam ilitolewa kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya awali kushinda 2-0 katika mchezo wa kwanza nyumbani, Uwanja wa Azam Compex, Chamazi, Dar es salaam.

Kwa upande wa Yanga SC wao wanatarajia kumenyana na Klabu ya FC Platnum ya Zimbabwe katika mzunguko wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika baada Yanga kuitoa BDF XI ya Botswana.

Yanga ilifungwa mabao 2-1 na BDF, Uwanja wa Lobatse na BDF na kuifanya isonge mbele kwa ushindi wa jumla ya 3-2 baada ya awali kushinda 2-0, Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Kwa upande wa FC Platnum ya Zimbabwe, iliifumua Sofapaka FC ya Kenya na kusonga mbele kwa jumla ya magoli 4-2. FC Platnum iliilaza Sofapaka 2-1 jana kwenya mechi ya mkondo wa pili iliyosakatwa Uwanja wa Mandava Mjini Zvishavane, Zimbabwe.

Mshambuliaji wa Sofapaka Mburundi Fiston Abdoul Razak aliipa timu yake uongozi katika dakika ya nne lakini Wisdom Mtasa akasawazisha mambo baada ya robo saa.

Timu zote zilipoteza nafasi za kuhesabu kabla ya mwamuzi wa katikati na Mbotswana Torelo Mositwane kupuliza kipienga kuashiria mapumziko.

Katika kipindi cha lala salama, Mtasa alicheka na nyavu dakika ya 54 na kuua matumaini ya vijana wa Kocha Sam Timbe kurejea mchezoni kwani walishindwa kufunga mabao manne ili kupenyeza awamu ijayo.