Thursday , 23rd Jun , 2016

Ni huzuni kwa Wasweden lakini pengine itakuwa ni furaha kwa mashabiki na kocha wa United Jose Mourinho kwa matokeo ya kipigo kwa timu ya taifa ya Sweden jana usiku kwani sasa watakuwa na hamu ya kuona mshambuliaji Ibrahimovic akitua Old Trafold

Zlatan Ibrahimovic akiruka hewani kujaribu kufunga dhidi ya Ubelgiji.

Goli pekee lililofungwa na kiungo mkabaji Radja Nainggolan anayewaniwa na Chelsea,limeifurusha katika michuano ya Euro timu ya Sweden ya Zlatan Ibrahimovic katika michuano hiyo inayoendelea huko nchini Ufaransa ambayo sasa inafikia katika hatua ya 16 bora.

Kipigo hicho ni kama kifo cha nzige na furaha kwa kunguru ambapo sasa klabu ya Manchester United chini ya Mreno Jose Mourinho ni kama wataokota dodo baada ya kuwepo na mazungumzo ya awali juu ya mshambuliaji Zlatan ambaye alikuwa amwage wino kabla ya kuanza michuano hiyo lakini ikashindikana na yeye mwenyewe kudai atafanya hivyo baada ya kuhitimishwa kwa michuano hiyo.

Na sasa ni wazi kocha Mreno Jose Mourinho atahitaji mshambuliaji huyo mrefu mwenye miaka 34 afike jijini Manchester kukamilisha dili la usajili wake na kuanza kazi mara moja wakati mkufunzi huyo akiwa tayari kuanza programu za maandalizi ya msimu mpya wa wanshindano mbalimbali ya ndani na nje huku akianza msimu mpya wa ligi kuu ya England EPL kwa mchezo dhidi ya Bournemouth mwezi Agasti mwaka huu.

Zlatan anatua United kama mchezaji huru baada yakumaliza mkataba wake na matajili wa Ufaransa timu ya Paris St. German [PSG] na kutokana na umri kwa na kwa sheria za Uingereza katika soka hasa ligi kuu mchezaji anayezidi miaka 33 huwa anapewa mkataba wa mwaka mmoja au chini ya hapo.

Kwa ushindi huo Ubelgiji imesonga mbele hatua ya 16 Bora na kumwacha mshambuliaji nyota na nahodha wa Sweden, Zlatan Ibrahimovich na kikosi chake, wakirejea kwao Ulaya Kaskazini.

Mechi ilikuwa tamu na ya kuvutia, lakini mwisho Sweden wanafunga safari kurejea kwao baada ya kipigo hicho cha bao 1-0.