Beki Taifa Stars Oscar Joshua akikabiliana na mchezaji wa Malawi katika mechi ya kirafiki jijini Mbeya
Taifa Stars na Malawi (Flames) zinapambana Jumanne (Mei 27 mwaka huu) katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 11 jioni.
Mechi hiyo itakuwa ya mwisho kwa Taifa Stars kujipima kabla ya kucheza mchezo wa marudiano wa michuano ya Afrika na Zimbabwe (Mighty Warriors) utakaofanyika Juni Mosi mwaka huu jijini Harare.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ipo kambini Tukuyu mkoani Mbeya chini ya Kocha wake Mart Nooij kujiandaa kwa mechi dhidi ya Malawi na ile ya Zimbabwe.
Malawi imewasili leo mchana (Mei 24 mwaka huu) kwa ndege ya Malawian Airlines kwa ajili ya mchezo huo ikiwa na msafara wa watu 27, na imefikia kwenye hoteli ya Sapphire Court iliyopo Mtaa wa Lindi jijini Dar es Salaam.
Flames inayofundishwa na mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Malawi, Young Chidmozi inatarajia kufanya mazoezi leo jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Baada ya mechi hiyo, Malawi itakwenda moja kwa moja nchini Chad kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika itakayochezwa Mei 30 mwaka huu jijini Ndjamena.