
Mechi ya Simba Vs Polisi Dar
Polisi Dar iliikatia rufaa Simba SC kwa kumtumia beki wake, Novaty Lufunga katika mchezo wa kombe la TFF, maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) hatua ya 32 Bora Jumapili, Uwanja wa Uhuru, Dar rs Salaam.
Katika mchezo huo ambao Simba ilishinda 2-0, mabao ya Pastory Athanas kipindi cha kwanza na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kipindi cha pili, Lufunga alikuwa benchi kama mchezaji wa akiba muda wote mchezo.
Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas amesema kwamba Rufaa ya Polisi haikusikilizwa kabisa kwa sababu timu hiyo haikukamilisha taratibu.
“Polisi walifanikiwa kukata rufaa yao ndani ya muda, lakini bahati mbaya kitu kimoja tu, hawakulipa ada, hivyo rufaa yao haikusikilizwa kwa kuwa ilikuwa ipo kinyume cha utaratibu,”alisema Lucas.
Pamoja na hayo, Msemaji huyo wa TFF akasema kwamba hata kama rufaa hiyo ingesikilizwa Polisi Dar wasingeshinda kwa sababu kanuni za Kombe la ASFC hazikuwazuia Simba kumtumia mchezaji huyo.
Akifafanua, Lucas alisema kwamba adhabu zote za michuano hiyo hufanya kazi katika msimu husika pekee na kwamba katika kila msimu mpya mambo huanza upya.