Saturday , 8th Nov , 2014

Baada wa kupoteza michezo yao iliyopita wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, timu za Yanga na Azam za jijini Dar es salaam, leo zimeibuka na ushindi katika mechi zao na kutwaa pointi 3 muhimu.

Simon Msuva

Kiungo machachari wa Yanga, Simon Msuva leo ameibuka shujaa baada ya kuifungia timu yake mabao mawili muhimu dhidi ya Mgambo JKT na kuipa ushindi muhimu wa 2-0.

Msuva ambaye ameingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Niyonzima, ameikuta timu yake ikiwa imeelemewa kwa kiasi kikubwa na maafande wa Mgambo JKT, lakini aliweza kubadilisha kabisa sura ya mchezo na kuipa Yanga uhai.

Msuva amefunga mabao hayo dakika za 74 na 90.

Katika uwanja Manungu Morogoro mechi kati ya Mtibwa Sugar na Kagera Sugar imevunjika baada ya kumalizika kwa dakika 45 za Kipindi cha Kwanza kutokana na uwanja kujaa maji kutokana na mvua kubwa iliyonyesha leo.

Kwa mujibu wa msemaji wa Mtibwa Thobias Kifaru pambano hilo litamaliziwa kesho Novemba 9, 2014 saa 2.00 asubuhi kwa kucheza dakika 45 zilizobakia.

Matokeo ya mechi nyingine ni haya:-

Azam FC 2 –1 Costal Union
Stand United 1 - 0 Mbeya City
Polisi Moro 1 - 0 Tanzania Prisons (Danny Mrwanda, 72)