
Akizungumza jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa mashindano wa Shirikisho la Soka nchini TFF, Boniface Wambura amesema timu hizo ni zile zilizofuzu katika mechi za awali ambapo Kagera inatarajia kukutana na Mwanza Uwanja wa Bukoba, Arusha itakutana na Tanga mechi itakayochezwa Arusha, Pwani na Kinondoni uwanja wa Mabatini, ilala na Mtwara Uwanja wa Karume jijini Dar es salaa, Katavi na Mbeya Uwanja wa Katavi huku Ruvuma na Iringa zikikutana Januari 19.
Wambura amesema, mechi baina ya Shinyanga na Simiyu ilivunjika katika Dakika ya 70 ambapo Kamati ya maendeleo ya Mpira wa Miguu ya wanawake ilipitia ripoti na kugundua kuwa mwamuzi wa mechi hiyo alivunja kimakosa huku mwamuzi wa mezani akiwa na nafasi ya kuendeleza mechi.
Wambura amesema kwa ripoti zote zinazohusiana na mechi hiyo, kamati imeona kuwa Katibu wa Chama cha Mpira Mkoani Simiyu Emmanuel Sologo alihusika na vurugu zilizopelekea kupigwa kwa mwamuzi wa mechi hiyo ambapo suala lake linafikishwa katika kamati ya nidhamu ya TFF kwa hatua zaidi huku Kocha wa Timu ya Simiyu Emmanuel Babu ambaye pia alichangia katika vurugu ambaye amesimamishwa kuifundisha timu hiyo.
Wambura amesema, kamati pia imewaondoa Kamishna wa mechi pamoja na mwamuzi kuendelea na mechi hizo ambazo vurugu zake zimeathiri michuano hiyo.
Wambura amesema, mechi nyingine iliyovunjika ni Dodoma na Singida ambapo katika mechi ya Marudiano iliyotarajiwa kuchezwa Singida Timu ya Singida haikufika Uwanjani huku Kaimu katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoani Singida Gabriel Gunda akihusika kwa timu kutoingia uwanjani ambapo kamati imemfungia kwa miaka miwili kutojihusisha na Mpira.