Tuesday , 17th Mar , 2015

Ligi Kuu ya Vodacom inatarajiwa kuendelea kesho kwa viwanja vitatu kutimua vumbi ambapo Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Yanga watawakaribisha Kagera Sugar mchezo utakaoanza majira ya saa 10 kamili jioni.

Akizungumza na East Africa Radio, Kocha wa Kagera Sugar Jackson Mayanja amesema, hana wasiwasi na timu hiyo na hawachezi mpira na mchezaji mmoja mmoja wa Yanga bali wanacheza na Kikosi kizima cha Yanga na pia wanacheza mpira wa pamoja.

Mayanja amesema, mpaka sasa anakiamini kikosi chake japo anamchezaji mmoja Abuu Mtiro ambaye ni Majeruhi lakini wachezaji waliobaki watasaidia timu hiyo kuibuka na ushindi katika mechi ya kesho.

Kwa upande wa Yanga, Mkurugenzi wa Kitengo cha Habari na mawasiliano wa Klabu hiyo, Jerry Muro amesema, kikosi kimeandaliwa vizuri kwa ajili ya mechi hiyo ambayo watawakosa wachezaji sita ambapo wanne wanatumikia adhabu ya kadi na wawili wakiwa ni majeruhi.

Jijini Tanga maafande wa Mgambo Shooting watakuwa wenyeji wa Simba SC katika mchezo utakaofanyika uwanja wa Mkwakwani, huku jijini Mbeya wenyeji Mbeya City watawakaribisha timu ya ya Stand United kutoka mkoani Shinyanga kwenye uwanja wa Sokoine.