Tuesday , 10th Apr , 2018

Klabu ya soka ya Azam FC imeweka wazi hali ya mshambuliaji wake Shaaban Idd ambaye alianguka kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mbeya City siku ya jumapili.

''Shabaan Idd anaendelea vizuri na amerejea na timu jijini Dar es salaam jana jioni chini ya uangalzii mzuri wa madaktari wa timu ambao wamehakikisha afya yake imeimarika kwani hakupata madhara makubwa sana'', imeeleza taarifa ya Azam FC.

Mshambuliaji huyo alianguka wakati mchezo ukielekea ukingoni akiwa anaelekea kwenye benchi baada ya nafasi yake kuchukuliwa na Joseph Kimwaga, hali ambayo ilipelekea kukimbizwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mbeya. 

Madaktari walieleza kuwa tatizo lililomkuta Idd ni kifua kumbana ghafla kutokana na hali ya baridi ya mkoani Mbeya haswa kutokana na mvua iliyonyesha wakati mchezo huo ukiendelea.

Azam FC tayari ipo jijini Dar es Salaam ikijiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Ruvu Shooting utakaofanyika Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani Alhamisi ijayo. Azam FC na Mbeya City zilitoka suluhu.